Kasulu, Tanzania
Serikali kupitia Mradi wa BOOST imepiga hatua kubwa katika kuboresha elimu ya awali nchini, kwa kuimarisha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji, pamoja na miundombinu na upatikanaji wa zana za kufundishia.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi la ufuatiliaji lililohusisha Maafisa wa Uthibiti Ubora wa Elimu kutoka Halmashauri ya Mji Kasulu pamoja na Ofisi ya Mawasiliano Serikalini, Afisa Elimu ya Awali na Msingi Bw. Julius Buberwa alisema kila shule ya msingi sasa ina darasa la elimu ya awali, hivyo kila mwanafunzi anayeanza shule ya msingi anakuwa tayari amepitia msingi huo muhimu wa awali.
Katika juhudi hizo, serikali kupitia mradi huo imefanikiwa kujenga madarasa ya mfano katika shule tano za Murusi, Bajana, Juhudi, Kidyama na Mumnyika. Buberwa alisema madarasa hayo yameleta mabadiliko makubwa kwa kuongeza mvuto wa elimu ya awali na kusababisha ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa katika shule za serikali ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
“Madarasa haya si tu yameboresha mazingira ya ujifunzaji, bali pia yameongeza hamasa kwa wazazi kupeleka watoto wao shule,” alisema Buberwa.
Pamoja na ujenzi wa miundombinu, walimu wa madarasa ya awali wamepewa mafunzo mahsusi juu ya mbinu bora za kufundisha na namna ya kutumia zana za kufundishia. Mafunzo hayo yameleta maboresho makubwa darasani kwa kuifanya elimu ya awali kuwa ya kuvutia na rahisi kueleweka kwa watoto. Katika kuimarisha matumizi ya zana hizo, serikali kupitia Halmashauri ya Mji Kasulu imepeleka fedha kwa ajili ya utengenezaji wa zana za kufundishia kwa shule mbalimbali.
Katika kipindi cha awamu ya kwanza, shule 10 zilipokea kiasi cha Shilingi 585,500/= kila moja, na kwa awamu ya pili, shule 29 zimepokea Shilingi 675,000/= kila moja. Bw. Buberwa alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuleta mageuzi chanya katika sekta ya elimu. “Shule za serikali sasa zinaonekana bora, na tofauti kati ya shule za umma na binafsi inaendelea kupungua,” aliongeza.
Mradi wa BOOST umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya elimu ya awali nchini kwa kuhakikisha kuwa watoto wanapata fursa sawa ya kuanza elimu katika mazingira salama, rafiki, na yaliyoandaliwa kitaalamu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mwl Vumilia J. Simbeye amemshukuru kwa dhati Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya Sekta ya Elimu Msingi na Sekondari Nchini Tanzania kupitia Miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ile ya BOOST na SEQUIP.
____________________________________