Ameyaeleza hayo leo wakati akifungua rasmi kikao cha wajumbe wa balaza la wazee na watu wenye ulemavu Halmashauri ya Mji Kasulu kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri na kuwahusisha viongozi mbalimbali wa wa vyama vya walemavu na wawakilishi wa wazee.
Katika kikao hicho kilichoratibiwa na Halmashauri ya Mji kwa ufadhiri wa Shirika lisilo la kiserikali HelpAge Tanzania Katibu tawala Bi Teresia Mtewele ameonya tabia ya baadhi ya wazazi kutowapa thamani sawa watoto wenye ulemavu na kuwatenga au kuwaficha kwa kuona kama laana kuzaa watoto wenye hali hizo.
Mtewele amesema Serikali imeweka mipango Madhubuti ya kudhibiti vitendo vya ukatili kwa watu kutoka makundi maalum na kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia makundi haya katika Nyanja mbalimbali ikiwemo afya Pamoja na elimu.
Aidha Katibu tawala huyo ameionya tabia ya baadhi ya wazazi kuwafanya watoto wenye ulemavu kitega Uchumi na kuwatembeza huku na kule wakiomba msaada badala yake wawasaidie kwa kuwawezesha kupata haki zao za msingi kwani wanaweza kutimiza ndoto zao kama watoto wengine
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama Vya Walemavu Kasulu Zakayo Nkohozi
ameishukuru serikali kwa namna inavyoendelea kuwakumbuka na kuwashirikisha watu wenye mahitaji maalum katika shughuli mbalimbali na kuwapatia msaada mbalimbali kutatua changamoto wanazopitia ikiwemo kuwapatia vifaa wezeshi. Aidha amesema huko nyuma walemavu walipuuzwa na kuonekana hawana uwezo wa kufanya chochote lakini serikali inaendelea kuwapa mafunzo yanayowawezesha kujitambua na kujihusisha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazowawezesha kupata kipato na hivyo kujikimu kimaisha badala ya kuomba omba mitaani.
Kwa upande wake Afisa Ustawi Wa jamii Ndugu Festo Pansian Solly amesema kumekuwepo na changamoto ya makundi ya wazee na watu wenye ulemavu kutokujua sera, miongozo na sheria zinazo wahusu na kuongeza kwamba wazee na watu wenye ulemavu haya ni makundi yanayoshabihiana hasa kwenye changamoto zao na hivyo yanahitaji uangalizi wa kipekee hivyo,halmashauri kwa kulijua hili imeona ni vyema kuyakutanisha makundi haya na kuwapitisha katika kuwaelekeza majukumu yao Pamoja na kuweka mpango mkakati wa namna ya kuhuisha mabalaza yatakayowawezesha kutatua changamoto zao.
Restituta Damiano mwakilishi kutoka Shirika la HelpAge Tanzania mkoa wa Kigoma ameishukuru Serikali kupitia Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Kasulu kwa namna wanavyowawezesha kufanya shughuli zao za kuwawezesha wazee na watu wenye ulemavu kujitegemea katika kufanya shughuli zao za kujikimu kimaisha na kuondokana na utegemezi unaopelekea kundi kubwa la ombaomba