Mwl. Vumilia Simbeye aleta mapinduzi Kasulu Mji! Kwa mara ya kwanza, timu rasmi za michezo za watumishi wa Halmashauri ya Mji Kasulu zimeanzishwa. Afya, mshikamano, na vipaji sasa vinawekwa mbele.
Afisa Michezo wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Bw. Daudi Schinga, amesema leo wamekusanyika katika viwanja vya Kiganamo kwa ajili ya kuanza rasmi maandalizi ya timu ya halmashauri hiyo. Aidha, siku ya Ijumaa kutakuwa na mechi ya kirafiki kati ya Halmashauri ya Mji Kasulu na Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, itakayofanyika katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Kasulu. Ameushukuru uongozi wa Mkurugenzi Simbeye kwa wazo hili la kuunganisha watumishi kupitia michezo, akibainisha kuwa timu hiyo itasajiliwa rasmi na kushiriki mashindano mbalimbali ndani na nje ya mji, chini ya mlezi wake ambaye ni Mkurugenzi mwenyewe.
Mkurugenzi Simbeye amewataka watumishi wote kushiriki kikamilifu katika mazoezi na mashindano hayo, akisisitiza kuwa michezo ni sehemu muhimu ya maendeleo ya kiutendaji na kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Halmashauri ya Mji Kasulu, hatua hii ni sehemu ya mpango mpana wa kuimarisha sekta ya michezo na kuibua vipaji vipya miongoni mwa watumishi wa umma.
Wafanyakazi wa Halmashauri ya Mji Kasulu wamepokea kwa furaha hatua hii, wakieleza matumaini kuwa itachangia kuimarisha afya na mshikamano miongoni mwa watumishi, na pia kuleta heshima kwa halmashauri yao katika mashindano ya kitaifa.
Kwa upande wake, Kocha wa timu ya netiboli ya watumishi, Mwl. Siyonkile Wilson Mnyampara, amepongeza hatua ya Mkurugenzi Simbeye na kueleza kuwa ari na morali ya wachezaji iko juu. Ameahidi kuwa kwenye mashindano ya kitaifa ya watumishi wa umma, timu yao ya netiboli itaweka historia kwa kurudi na kombe.