Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Bw. Vumilia J. Simbeye, ameendelea kuwa kielelezo cha vitendo kwa kuongoza zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika leo katika maeneo mbalimbali ya mji, kama ilivyo ada kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Akizungumza baada ya zoezi hilo, Bw. Simbeye amesema kuwa mwitikio wa wananchi na watumishi wa Halmashauri unaongezeka siku hadi siku, na leo idadi kubwa zaidi ya washiriki imejitokeza ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Ametoa wito kwa wadau na taasisi zote kuungana katika jitihada hizi kila mwezi ili mji uwe safi na wenye kuvutia, huku akisisitiza kauli mbiu:
“Usafi unaanza na mimi.”
Mkurugenzi huyo pia amefafanua kuwa Halmashauri imeingia mkataba na kikundi cha vijana kwa ajili ya ukusanyaji taka, kikundi ambacho kilipatiwa mkopo wa Shilingi milioni 60 kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani. Vijana hao wameweza kununua bajaji guta ambazo zimefanikisha ukusanyaji wa taka hadi vichochoroni ambapo magari makubwa hayawezi kufika. Hatua hii ni utekelezaji wa azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Kwa kuonyesha mfano bora, Bw. Simbeye alishiriki mwenyewe kwa kushika vifaa vya usafi na kufanya kazi bega kwa bega na wananchi na watumishi wa Halmashauri, jambo lililoleta ari kubwa kwa washiriki wote.
Aidha, amesisitiza kuwa Halmashauri imejipanga kushiriki kikamilifu katika matukio makubwa yajayo ikiwemo Nanenane, Mwenge wa Uhuru na Uchaguzi Mkuu