Kasulu, 24 Julai 2025
Waziri wa Maji, Mh. Jumaa Hamidu Aweso (MB), amefurahishwa na maendeleo makubwa ya mradi wa maji wa Miji 28 unaotekelezwa katika Halmashauri ya Mji Kasulu.
Mradi huo, ambao umefikia asilimia 49 ya utekelezaji, unakadiriwa kugharimu TSh bilioni 35 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2025. Ukikamilika, utahudumia kata 12 kati ya 15 za mji huo, na kuondoa kabisa changamoto ya maji kwa wakazi wa Kasulu Mjini na mitaa yake.
Chanzo cha maji kinapatikana katika Mto Ruchugi – Kata ya Msambara, ambapo mradi unatekelezwa na Kampuni ya MEGHA MAIL kutoka India chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kasulu (KUWSSA).
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Bi. Neema Marco wa Msambara alisema:
“Naona kama muujiza! Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu mkubwa.”
Waziri Aweso alitoa maagizo kwa Mkuu wa Wilaya Isaack Mwakisu kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, huku akimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujitoa kwake kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya maji safi.
Tukio hilo limeshuhudiwa na mamia ya wananchi waliojitokeza kwa shangwe, pamoja na viongozi mbalimbali wa wilaya na mkoa.