Ikiwa zimebaki siku nne kuelekea siku ya uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa Novemba 27,2024 Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Mji Kasulu Mwalimu Vumilia Simbeye amewaasa wasimamizi wa vituo Makarani waongozaji,Wasimamizi wa Kata, Wasimamizi wa Mitaa na Makarani wa akiba wakiwa ni watumishi wa Umma kuzitunza vyema nafasi zao kuwa na nidhamu ya hali ya juu na kuiheshimisha Serikali wakati wakisimamia zoezi na upigaji kura linalotegemewa kufanyika siku ya Jumatano kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa kumi alasiri.
Hayo ameyasema wakati wa ufunguzi wa semina ya maelekezo kwa wasimamizi wa vituo na waongozaji wa wapiga kura wanaotarajiwa kushiriki kwenye zoezi hili.
Mwalimu Simbeye amewataka wapokee maelekezo kwa umakini zaidi na kuwataka wanasemina hao kuwa na lugha moja ili kuiheshimisha Serikali ya Muungano wa Tanzania na kufanikisha zoezi lililobakiza siku nne.
Aidha amesema zoezi hili la uchaguzi ni kwa mujibu wa misingi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Uchaguzi huu hufanyika kila baada ya miaka mitano huku Vyama vinavyoshiriki uchaguzi huu wa Serikali za mitaa ni Pamoja na CCM ,CHADEMA, CUF ,ACT WAZALENDO, NCCR MAGEUZI ,SAU, na TLP.
Katika Halmashauri ya Mji Kasulu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika katika vituo maalumu mia moja kumi na nane(118) vilivyopangwa vya kupiga kura hivyo amewataka kusimamia vituo hivyo kwa umakini wa hali ya juu ili wananchi waweze kutimiza azma yao ya kuwachagua viongozi watakaoowangoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Naye mshiriki wa semina hiyo Tatu Mussa Sabagi ambaye ni msimamizi msaidizi ngazi ya Mtaa kwa niaba ya wenzake amesema “Tuko tayari kufuata maelekezo tuliyopewa kwa ueledi wa hali ya juu tunaimani zoezi hili litakwenda vizuri sana”