SHULE YA MSINGI NYANSHA KUNUFAIKA NA MADAWATI KUTOKA SHIIKA LA POSTA TANZANIA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana ,Ajira na wenye Ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini Prof.Joyce Lazaro Ndalichako amelishukuru shirika la posta Tanzania kwa kutoa madawati kwa shule ya msingi nyansha kwani hii itasaidia kuendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za kasulu mjini.
Aliyasema hayo wakati wa zoezi la ugawaji wa madawati hayo na kusema,”Serikali itaendelea kutatua changamoto za uhaba wa madawati katika shule zote zilizopo katika halmashauri ya Mji Kasulu niwaombe viongozi wa serikali kutumia ipasavyo pesa zinazotolewa na serikali kwa ajili ya shughuli za maendeleo na iwapo hamtasimamia miradi ya maendeleo kwa weledi mtalisababishia Taifa hasara na kuchelewesha maendeleo
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa masoko na mahusiano kutoka shirika la posta Tanzania Bw.Amos millinga amesema kuwa lengo la kugawa madawati hayo ni kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto na wanafunzi ili kutimiza ndoto zao katika kupata elimu.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu amesema,”nawaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kujitokeza kusaidia miundombinu mashuleni hasa madawati kwani mpaka sasa wilaya ya kasulu inaupungufu wa madawati 22500 kwa shule za msingi pia nasisitiza muyatunze ili yadumu kwa muda mrefu”.
Mwakisu ameendelea kusema kupititia hadhara hii nitoe rai yangu wananchi kujiepushe na maswala ya Kamchape kwani si ya kweli na yako kwa lengo la kuchonganisha jamii na kuwarudisha kimaendeleo kwa kuwachukulia mali zao.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bi Telidesa Kuka baada ya kupokea madawati amesema,”tunawashukuru sana shirika la posta kwa madawati haya kwani yanakwenda kumaliza kabisa changamoto ya uhaba wa madawati iliyokuwepo hapo awali na pia itasaidia kupunguza utoro na kuongeza ufaulu wa watoto shuleni hapa”.
Jumla ya madawati 100 yenye thamani ya shillingi million 9860 000 yametolewa na shirika la posta Tanzania kwa shule ya msingi Nyansha iliyopo kata ya nyansha halmashauri ya mji kasulu ikiwa ni juhudi za wadau wa maendeleo kuendelea kuunga mkono serikali kwa kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.