Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Bw. Nurfus Aziz Ndee, amewataka viongozi wa dini na watu maarufu kutumia nafasi zao na ushawishi walionao kutoa elimu na kukemea vitendo vya ukatili ili kujenga jamii iliyo salama.
Wito huo umetolewa leo wakati wa ufunguzi wa kikao cha kuwawezesha viongozi wa dini na watu maarufu, kilichoandaliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii – Kitengo cha Jinsia, kwa ufadhili wa UNICEF. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Ndee aliwaasa washiriki kushiriki kikamilifu na kuwa wazi katika kufichua matendo ya ukatili yanayotokea katika jamii ili sheria ichukue mkondo wake. Aidha, aliwaomba viongozi wa dini kutoa elimu juu ya vitendo vya ukatili na kukemea vitendo hivyo, sambamba na kufundisha waumini wao kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Serikali, ili kufanikisha lengo la kuwa na jamii iliyo salama.
Kikao hicho kinalenga kuwawezesha viongozi wa dini na watu maarufu kufikisha elimu ya kutokomeza vitendo vya ukatili katika jamii, hasa katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla. Aidha, ilielezwa kuwa si wananchi wote wanaofika katika maeneo ya ibada, hivyo kuwashirikisha watu maarufu ni njia muhimu ya kuwafikia wasiosali kupitia ushawishi wao katika jamii. Vilevile ilibainishwa kuwa si wote wanaofanya ukatili wana uelewa wa kutosha kuhusu madhara ya vitendo hivyo.
Akitoa maelezo, Afisa Maendeleo ya Jamii, Olivia Kasindu Thadeo, amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau inalenga kujenga jamii isiyo na ukatili ili kuongeza uzalishaji na kuleta maendeleo. Alisisitiza kuwa familia zikipona, jamii nzima itapona. Aliongeza kuwa pamoja na kikao hicho, juhudi nyingine zinaendelea ikiwemo mikutano ya hadhara, utoaji wa elimu mashuleni na katika jamii.
Katika kikao hicho, washiriki walielimishwa kuhusu aina mbalimbali za ukatili ikiwemo ukatili wa kipigo, kingono, kiuchumi, kutelekezwa na kisaikolojia, huku Mkoa wa Kigoma ukitajwa kuwa miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na changamoto ya vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mchungaji wa FPCT Murusi Kasulu, Thomas Masama, aliushukuru uongozi wa Halmashauri kwa kuandaa kikao hicho na kusema mapambano dhidi ya ukatili yanahitaji ushirikiano wa wazazi, viongozi na jamii nzima, na si kuachwa kwa Serikali pekee. Alitoa wito vikao kama hivyo viendelee kufanyika na kusisitiza umuhimu wa utekelezaji wake.
Naye Kuruthum Abdallah Bishehat wa Msikiti Jabarhila Kata ya Murusi alisema mafunzo hayo yamemjengea uelewa mkubwa, hususan kwa wanawake, akisisitiza umuhimu wa wazazi kukaa na watoto wao na kuwapa elimu ya kujilinda dhidi ya hatari. Alieleza kuwa mwanamke ni nguzo ya familia, na akisimama vizuri katika nafasi yake, jamii nayo itasimama. Pia alipendekeza tathmini ifanyike kila baada ya miezi mitatu ili kupima matokeo ya elimu inayotolewa na viongozi wa dini kuhusu matendo ya ukatili.