Hayo yamesemwa Leo hii na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu wakati akifunga mafunzo ya waalimu wa darasa la awali, darasa la kwanza na darasa la pili yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Murusi. Mafunzo hayo yaliwahusisha waalimu 32 kutoka halmashauri zote za mkoa wa Kigoma na yamefadhiliwa na wadau wa elimu wa mpango wa Shule Bora.
Katika hotuba yake ya kufunga, Mkurugenzi aliwashukuru wafadhili wa mpango wa Shule Bora kwa kuwezesha mafunzo haya muhimu,
"Nianze kwa kupongeza viongozi na waratibu wa Programu ya Shule Bora kwa kuendelea kuiunga mkono jitihada za za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu katika kuendelea kutambua umuhimu wa Sekta ya Elimu Nchini kupitia mpango wa Shule Bora kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa KKK kwa darasa la kwanza na la pili, Hisabati na Kiingereza." Alieleza Mkurugenzi Simbeye. Aliendelea kusisitiza umuhimu wa kuongeza ubunifu katika kufundisha ili kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu. Alieleza kuwa serikali inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha elimu na kuwaomba waalimu waendelee kubeba maarifa waliyopata kwa ubunifu zaidi katika kutumia zana na mbinu za kufundishia.
“Mafunzo haya ni fursa adimu ambayo mliyopata, nayo ibebeni kwa moyo mmoja na muendelee kuleta ubunifu mkubwa katika darasani. Elimu si jukumu la mwalimu pekee, bali ni jukumu la kila mmoja wetu kuleta maendeleo,” alisema Mkurugenzi.
Mwalimu Vumilia Msukuma, mkufunzi mkuu wa mafunzo, alisema kuwa walijifunza mbinu mbalimbali zitakazowasaidia kuwahudumia watoto kwa ufanisi zaidi na kuandaa mpango wa mafunzo wa kuendeleza uwezo wa waalimu katika shule.
Washiriki kutoka halmashauri za Kasulu na Kibondo walielezea umuhimu wa mafunzo hayo na kuomba usaidizi wa wazazi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Mkufunzi Hapinnes Peter kutoka Chuo cha Ualimu Singachini Moshi aliwasisitiza waalimu umuhimu wa kutumia michezo na nyimbo katika kufundisha stadi za msingi za KKK (Kiswahili, Hisabati na Kiingereza) ili kuondoa changamoto na kuongeza ufaulu katika mitihani.
Mafunzo haya ni sehemu ya jitihada za serikali na wadau wa mpango wa Shule Bora, mpango wa kitaifa unaolenga kuboresha ubora wa elimu kwa kuwekeza kwenye mafunzo ya walimu, vifaa vya kufundishia, na mazingira bora ya masomo ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na kujiendeleza kikamilifu