Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Bw. Daniel Kaloza, ameendelea na zoezi la kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi ambapo leo ametembelea vyuo vya elimu ya kati vilivyopo mjini Kasulu. Vyuo vilivyotembelewa ni pamoja na Chuo cha Ualimu Kabanga, Chuo cha Ualimu Kasulu na Chuo cha Ufundi FDC. Ziara hiyo imefanyika kwa kushirikiana na timu ya wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya halmashauri pamoja na maafisa habari.
Katika hotuba yake, Bw. Kaloza amewasisitiza wanafunzi kuhusu umuhimu wa kujitokeza kupiga kura na kuzingatia taratibu za kisheria siku ya uchaguzi ili kulinda amani ya nchi. Ameonya vijana kutokutumiwa na wanasiasa wenye malengo ya kujinufaisha binafsi kwa kuanzisha vurugu, na badala yake amewataka kuwa mabalozi wa amani na mshikamano katika kipindi chote cha uchaguzi.
Aidha, Bw. Kaloza amebainisha kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imezingatia makundi maalum kwa kuyawekea mazingira rafiki ya kupiga kura. Ametolea mfano watu wasioona ambao wameandaliwa karatasi maalum za kura zenye maandiko ya nukta nundu, wafungwa watakaopiga kura wakiwa magerezani, pamoja na makundi mengine ambayo yatapewa nafasi sawa kushiriki. Amesisitiza kuwa hakuna kundi litakaloachwa nyuma katika mchakato huu wa kidemokrasia.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mwanafunzi Masalu Chama kutoka Chuo cha Ualimu Kabanga ameeleza kuwa wametiwa moyo na elimu waliyoipokea na wamejipanga kuwapuuza wanasiasa watakaokuja kwa lengo la kuwatumia. Aidha, aliongeza kuwa elimu hiyo imewapa hamasa kubwa ya kushiriki uchaguzi kwa amani na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.
Elimu ya mpiga kura inaendelea kutolewa pia katika kata mbalimbali za Halmashauri ya Mji Kasulu ambapo wananchi wanapata nafasi ya kuuliza maswali na kupata uelewa wa kina kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi. Hatua hii inalenga kuhakikisha kila mmoja anashiriki kikamilifu na kwa amani katika zoezi la kidemokrasia linaloendelea nchini.
"Kura yako Haki yako Jitokeze Kupiga Kura"