Leo, Halmashauri ya Mji wa Kasulu imekabidhi mikopo yenye jumla ya Shilingi 433,647,000 kwa vikundi 32 vya Wanawake na Vijana, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa dirisha la pili la utoaji mikopo kwa mwaka 2024/2025.
Mikopo hiyo imetolewa kwa vikundi 25 vya Wanawake na vikundi 7 vya Vijana, ikihusisha wanufaika 230 waliopatiwa pia mafunzo ya ujasiriamali ili kuboresha shughuli zao.
Katika hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mji, Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, aliwasihi wanufaika kutumia mikopo hiyo kwa kufanya shughuli walizokusudia ili kuhakikisha marejesho kwa wakati, kwa lengo la kusaidia wananchi wengine kupata fursa hiyo.
Sambamba na utoaji wa mikopo, vifaa vya kuzolea taka vyenye thamani ya Shilingi 60,000,000 vilivyotolewa na kikundi cha wahifadhi wa usafi wa mazingira vilikabidhiwa rasmi kwa ajili ya kuboresha usafi katika viunga vya Mji wa Kasulu.
Pia, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kasulu, katika salamu zake, alieleza kuwa chanzo cha mikopo hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM. Alipongeza uongozi wa Halmashauri ya Mji Kasulu kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani, na akawaasa wananchi kujiandaa vyema kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo, huku akisisitiza kutojihusisha na vitendo vya rushwa.