Halmashauri ya Mji Kasulu imeendesha mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata, yakiwa ni maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni. Mafunzo hayo yamehusisha washiriki 30 kutoka kata 15, kila kata ikiwakilishwa na wasimamizi wawili.
Katika siku ya kwanza ya mafunzo, washiriki wote waliapishwa rasmi mbele ya Mheshimiwa Immaculate Shuli, Hakimu Mkazi Mwandamizi, wakiahidi kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu bila upendeleo wa kisiasa.
Mgeni rasmi, ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kasulu Mji, Ndugu Nurfus Aziz Ndee, aliwataka wasimamizi hao kutambua uzito wa jukumu walilopewa na kuwataka wasimamie mchakato wa uchaguzi kwa uadilifu, weledi na uzalendo. Aliwasisitiza kujiepusha na ushawishi wa kisiasa, kutokuwa sehemu ya kampeni au propaganda za vyama, na badala yake wawe walinzi wa amani na haki katika maeneo yao.
Aidha, aliwataka kusoma na kuelewa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria, kanuni na maelekezo mbalimbali ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Alikumbusha kuwa wao ni watumishi wa Tume kwa mujibu wa sheria, hivyo taarifa na maamuzi yoyote yahusuyo uchaguzi yatolewe kwa niaba ya Tume na si vinginevyo.
Mafunzo haya ni sehemu ya hatua madhubuti zinazochukuliwa kuhakikisha uchaguzi mkuu wa 2025 unakuwa wa amani, huru, haki na unaoaminika. Halmashauri ya Mji Kasulu inaendelea kusimamia maandalizi haya kwa karibu, ikiwa ni sehemu ya wajibu wake katika kulinda misingi ya demokrasia nchini.