WAZAZI MKOANI KIGOMA WATAKIWA KUWALINDA WATOTO ILI KUPUNGUZA UKATILI WA KIMTANDAO
Kutokana na wimbi la ukatili wa kijinsia unaoendelea kutokea mkoani kigoma wazazi na walezi wilayani kasulu wametakiwa kuacha tabia ya kuwamilikisha simu watoto wenye umri chini ya miaka 18 lengo ikiwa ni kuwalinda na vitendo vya ukatili mtandaoni.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa SMAUJATA Taifa Bw Sospeter Bulugu wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukatili na utoaji wa taarifa ndani ya masaa 72 iliyofanyikia katika viwanja vya umoja kata ya Murubona kasulu mjini na kusema,”takwimu zinaonyesha kuwa watoto wengi wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia mitandaoni na kwamba haoni sababu ya mzazi kumruhusu mtoto kumiliki simu kabla ya wakati”.
Kwa upande wake bi Beatrice Emmanuel kutoka shirika la IRC kitengo cha kupinga na kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana amesema,”ili kuwa na Taifa lenye haki ,Amani na maendeleo wanaendelea kutoa elimu kwa jamii lengo ikiwa ni kuokoa maisha ya watu ambao wamekuwa wakipoteza maisha kwa kufanyiwa vitendo vya kikatili”.
Aidha Mkurugenzi wa shirika la endeleza wazee Mkoa wa Kigoma Bi kokupima alisema,”wazee wamekuwa wakitendewa vitendo vya ukatili kama vipigo,ubakaji pamoja na kunyang’anywa mali katika maeneo yao na wanashindwa kutoa taarifa kutokana na uelewa mdogo wa Elimu ya namna ya kuripoti matukio ya kikatili.
Hata hivyo baadhi ya wanafunzi waliohudhuria uzinduzi wa kampeni hiyo kutoka shule ya sekondari Kinkati na Murubona wamesema,”wazazi wanalo jukumu la kuhakikisha wanawatimizia mahitaji yote watoto wao hili litawasaidia wao kutokuwa na tamaa ya kupokea zawadi kwa watu ambao sio wema”.