WAZIRI WANCHI OFISI YAWAZIRI MKUU KAZI AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU ASOMA BAJETI YA WIZARA HIYO YA MWAKA 2022/2023 YENYE LENGO LA KULETA USTAWI WA KIUCHUMI
Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu kazi,ajira na watu wenye ulemavu Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa serikali imeanza kutekeleza mpango wa utekelezaji wa kazi mbalimbali na miradi ya maendeleo ikiwemo kusimamia masuala ya kazi na wafanyakazi nchini.
Ameyasema hayo leo julai 3 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu nakuelezea mipango ya bajeti na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2022/2023 kuwa serikali ya awamu ya sita ya Raisi Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuleta ustawi wa kiuchumi na kusaidia watu wenye ulemavu kwa kujenga vyuo vipya vitatu vya ufundi stadi na kuvifanyia marekebisho vituo vinne ili wawe na uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Aidha Ndalichako amesema kujengwa kwa vyuo hivyo kupitia bajeti ya wizara yake pamoja na ukarabati unaofanywa kutasaidia kulifanya kundi kubwa la watu wenye ulemavu kuwa na taaluma ambayo ndiyo msingi katika kuajiriwa,kujiari au kuajiri watu wengine kwenye shughuli watakazoanzisha na pia bajeti hiyo inalenga kukuza ujuzi na utoaji wa ajira nchini ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.
Katika kuwajenga kuweza kufanya shughuli za kiuchumi vijana 22,200 wamepatiwa mafunzo ya ujuzi wa uana genzi, vijana 3600 watapatiwa mafunzo ya ujenzi na kilimo ya kitalu nyumba kwa mikoa mitano nchini, ambapo pia vijana 500 wamepatiwa mafunzo juu ya ujuzi wa uchumi wa bluu kupitia ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba na kujenga vituo vitano kwa vijana wanaopata mafunzo ya uanagenzi.
Hata hivyo Waziri ndalichako ameendelea kusema kuwa kuendana na hali hiyo serikali kupitia wizara yake itaifanyia mapitio sera ya Taifa ya huduma na maendeleo ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 ili kuweka mazingira mazuri kwa watu wenye ulemavu kushiriki shughuli za uchumi na mipango ya taifa.pamoja na utekelezaji wa mipango hiyo serikali imeanza kutekeleza mpango kabambe wa uwezeshaji kiuchumi kwa vijana kwa kuwapatia mafunzo na mitaji ili waweze kujiajiri na kutoa ajira kwa vijana wenzao.
Ndalichako amemalizia kwa kusema “mwelekeo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 unalenga ukusanyaji wa maduhuli,matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo ambapo katika mwaka wa fedha 2022/2023 Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Watu wenye ulemavu imepangiwa kukusanya Jumla ya shilingi bilioni 45 sawa na ongezeko la asilimia 33.3kutoka shilingi bilioni 30 mwaka wa fedha wa 2021/22.’’