Halmashauri ya Mji wa Kasulu leo imezindua rasmi uwanja mpya wa mchezo wa volleyball uliojengwa katika maeneo ya Ofisi za Utamaduni, hatua inayoashiria ari mpya ya kuinua michezo katika mji huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa uwanja huo, Afisa Michezo wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Bw. David Schinga, alisema uwanja huo umejengwa kutokana na mafanikio makubwa ambayo mchezo wa volleyball umekuwa ukipata katika mashindano mbalimbali.
“Tuliona ni vyema tuwe na uwanja maalum wa kisasa. Baada ya kumshirikisha Mkurugenzi wa Halmashauri, alikubali mara moja na akawezesha ujenzi huu kupitia mapato ya ndani,” alisema Bw. Schinga.
Aliongeza kuwa ujenzi wa uwanja huo ni uthibitisho wa dhamira ya halmashauri kuinua michezo na kutoa nafasi kwa vijana kuendeleza vipaji vyao.
“Tunamshukuru sana Mkurugenzi wetu kwa kujali michezo na kuwezesha vijana wetu kupata mahali pa kufanyia mazoezi,” aliongeza.
Katika bonanza hilo la uzinduzi, timu mbalimbali kutoka Kigoma Municipal Council, Buhigwe, Kasulu District Council na Uvinza zilishiriki, huku Kasulu Town Council ikiwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Kapteni wa Timu ya Buhigwe, Mhadhamu Muyenga, aliishukuru halmashauri kwa mwaliko na akapongeza jitihada zilizofanyika.
“Tumepata funzo kubwa kwa kuona uwanja huu. Nasi tutajitahidi kufanya kitu kama hiki katika halmashauri yetu,” alisema.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Michezo wa Kasulu Town Council, Bw. Emanuel Sonda, alitoa shukrani kwa Mkurugenzi kwa kujenga uwanja huo.
“Kabla ya uwanja huu tulikuwa na changamoto kubwa ya kufanya mazoezi. Sasa tuna furaha kubwa, tunampongeza Mkurugenzi kwa kuleta mabadiliko haya makubwa,” alisema Sonda.
Akizungumza wakati wa kufunga bonanza hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu aliwashukuru wageni wote kwa kushiriki na kusisitiza kuwa uwanja huo ni wa jamii nzima.
“Huu ni uwanja wa Kasulu Mji, lakini uko wazi kwa timu zote kutumia kwa mazoezi. Hii ni sehemu ya mikakati ya halmashauri kutumia mapato ya ndani kuendeleza michezo,” alisema Mkurugenzi.
Ameongeza kuwa halmashauri inaendelea kuweka mikakati ya kujenga viwanja vingine vya michezo ikiwemo netball na basketball, ili kuendeleza vipaji na kuimarisha afya za wananchi.