Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaack A.Mwakisu wakati akifungua mafunzo maalumu kwa watendaji wote wa kata zote za wilaya ya Kasulu pamoja na maafisa tarafa kwaajili ya kuwajengea uwezo na kuwakumbusha uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Katibu tawala,Mkuu wa Jeshi la Polisi,DC Mwakisu amesema sura ya serikali inaonyeshwa na watendaji katika maeneo yao ya kazi na hivyo ni vyema kuhakikisha wanatumika kwa weredi na uadilifu mkubwa katika utendaji wa shughuli zao za kila siku.
DC Mwakisu amekemea suala la baadhi ya watendaji kutoa vitisho kwa wananchi na kusema vitendo vya namna hii vinaondoa sifa nzuri ya serikali na kuwafanya wananchi wasiwe na ujasiri wa kueleza matatizo yao na hii kupelekea serikali kulaumiwa kutokana na kuwepo kwa migogoro mingi isiyotatuliwa.
Amesisitiza suala la ushirikiano na viongozi wengine wa serikali kama polisi kata na wengine na kusema kiongozi ni mtu anayeongoza wengine lakini pia naye anahitaji kuongozwa hivyo hauwezi kufanya kazi peke yako bila ushirika na watu anaowaongoza na pia kutoka kwa viongozi wengine.
Aidha DC Mwakisu amekemea suala la ‘’uboss ‘’katika maeneo yao ya kazi na kuwashauri wafuate maadili na kupendana na kuheshimiana wakimhudumia kila mtu kwa usawa na heshima pamoja na uadilifu.
DC amewatakia mafunzo mema na kuwataka wazingatie mafunzo yatakayotolewa na kwamba wanatakiwa kuhakikisha wanatekeleza yote watakayofundishwa kwa ajili ya ustawi wa jamii yetu na kuwapa imani wananchi kwa serikali yao inayofanya kazi kubwa kuwatumikia wananchi wao.
Suala la watendaji kukaa maeneo yao ya kazi ni suala ambalo pia DC Mwakisu amewaagiza na kusema ni jambo la msingi sana kiongozi kukaa eneo lake la kazi ili kuwapa uwezo wa kuyajua matatizo ya wananchi na hasa kwa mwaka huu wa uchaguzi "Nendeni mkakae katika maeneo yenu ya kazi achene kukaa mjini wakati wananchi wanahitaji kuhudumiwa,mtambue kwamba mmeaminiwa na Serikali kati ya watanzania wengi”.
Kwa upande wake Katibu tawala Wilaya ya Kasulu Bi Theresia Mtewele amewataka Watendaji na Maafisa Tarafa kujua mipaka ya uongozi na kuzingatia maadili ili kufikia malengo ya kinidhamu katika kudumisha utumishi wenye weledi, kujua mipaka ya uongozi na kuwa makini katika kufanya maamuzi hasa wakati wa utatuzi wa migogoro Kwa wananchi ili kujiepusha na migogoro baina ya mwajiri na Jamii wanayoihudumia.
Akitoa mada ya kwanza ya "Mjue Jirani yako" Afisa Uhamiaji Bi.Restuta amewashukuru watendaji wanaoendelea kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Uhamiaji na kuwaeleza kwamba wanategemea sana taarifa mbalimbali kama vile za wahamiaji haramu kutoka kwao na kuwaomba
Aidha bi Restuta amewataka watendaji kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa wakati wa kufanya operation yoyote inayohusiana na mambo ya uhamiaji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu na Jeshi la Uhamiaji.
Kwa upande wake SSP Athmani Issango OCD wilaya ya Kasulu akiwasilisha mada ya pili iliyohusu Ulinzi na Usalama amewataka watendaji kujua wajibu walionao na mamlaka yao kwa mujibu wa sheria katika kutekeleza majukumu yao hususani katika kusimamia ulinzi na usalama wa raia na mali zao ili kuepuka uvunjaji wa sheria.
Aidha ameshukuru ushirikaano unaoendelea kati ya jeshi la polisi na watendaji pamoja na maafisa tarafa katika kupambana na uhalifu na hivyo kufanya Wilaya ya Kasulu kuwa shwari na watu kuendelea kufanya kazi zao kwa amani.
Katika mafunzo hayo watendaji walipata wasaa pia kujifunza juu ya maada mbalimbali ikiwemo wajibu wa Serikali katika kupambana na kuzuia rushwa iliyowasilishwa na Alpha Eliatosha Afisa kutoka Takukuru ,Kanuni za utumishi wa umma ambayo iliwasilishwa na katibu tawala wa wilaya bi Theresia Mtewele pamoja na afisa utumishi Halmashauri ya Mji Kasulu Daniel Kaloza.