Katika kilele cha maadhimisho ya MEOS Day, watendaji wa mitaa wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu wamemkabidhi cheti cha pongezi Mkurugenzi wa Halmashauri, Mwl. Vumilia J. Simbeye, kama ishara ya kutambua mchango wake mkubwa katika kusimamia kwa weledi utendaji wa watumishi hao na kuiongoza halmashauri kwa ufanisi.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali ndani ya mji wa Kasulu yalijumuisha shughuli za kijamii na kiutamaduni, ikiwemo bonanza la michezo mbalimbali lililolenga kuimarisha afya na mshikamano miongoni mwa watendaji. Aidha, watendaji hao walitembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha Center of Hope ambapo walikabidhi msaada kwa watoto hao kama sehemu ya kujenga jamii yenye huruma na uwajibikaji.
Katika hafla ya usiku iliyohitimisha maadhimisho hayo, viongozi mbalimbali wa wilaya walihudhuria akiwemo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Ibrahim Mwangarume, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya. Pia walikuwepo wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi wengine wa serikali.
Akitoa salamu za serikali, Mwangarume aliwataka watendaji wa mitaa kuwa mabalozi wa maadili mema, hasa kwa vijana, akibainisha changamoto ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo imeikumba jamii kwa kasi. Aliwahimiza kuwa viongozi wenye heshima, ustaarabu na mfano bora wa kuigwa katika maeneo yao.
Aidha, aliwasisitiza kuongoza kwa kufuata Dira ya Maendeleo ya Taifa, kuibua miradi bunifu ya maendeleo, na kujiongezea maarifa ili waweze kuwaongoza wananchi kwa uelewa mpana na wa kisasa. Mwangarume alisifu ubunifu wa watendaji hao kuanzisha umoja wao maalum, akiwataka kuendelea kudumisha mshikamano na kuzijengea hamasa halmashauri nyingine kuiga mfano huo.
Katika tukio lilogusa mioyo ya wengi, watendaji wa mitaa walimkabidhi Mkurugenzi Simbeye cheti cha pongezi, wakimuelezea kuwa ni kiongozi mwenye maono, uwajibikaji na anayewajali watumishi wake. Walisema uongozi wake umewawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuimarisha utendaji katika ngazi za mitaa.
MEOS Day imeendelea kujidhihirisha kama jukwaa muhimu la kuonesha mshikamano wa watendaji wa mitaa na kuibua jitihada za kuboresha utumishi wa umma kwa manufaa ya jamii nzima ya Kasulu