Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Mh. Prof. Joyce (Mb) Ndalichako, amekabidhi gari la wagonjwa kwa Kituo cha Afya Mwamintare kilichopo Kata ya Heru Juu, Halmashauri ya Mji Kasulu. Makabidhiano hayo yalifanyika mbele ya wananchi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Halmashauri.
Waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mh. Ayubu Kilugu Garaba, Makamu Mwenyekiti, Mh. Hosea Gwanone Kayamba, na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwalimu Vumilia J. Simbeye, sambamba na wananchi wa Kata ya Heru Juu.
Gari hilo la wagonjwa lenye namba za usajili DFP 1113 linatarajiwa kuboresha utoaji wa huduma za dharura katika Kituo cha Afya Mwamintare, ambacho ni miongoni mwa vituo vya afya vinavyotoa huduma kwa wakazi wa Tarafa ya Heru Juu. Kituo hicho kimejengwa kupitia fedha za Serikali pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mji Kasulu.
Akizungumza na wananchi, Mh. Prof. Ndalichako alisema gari hilo litasaidia kwa kiasi kikubwa kusafirisha wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya Tarafa ya Heru Juu na maeneo mengine ya Halmashauri, hatua ambayo itapunguza rufaa zisizo za lazima na kuboresha usalama wa watoto wachanga na mama wajawazito.
Mbunge huyo alitoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zaidi.
Wananchi wa Kata ya Heru Juu pia walieleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakishukuru Serikali kwa kuwapatia gari la wagonjwa na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuboresha huduma za kijamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwalimu Vumilia Simbeye, alimpongeza Mbunge pamoja na Serikali, akisema kupokelewa kwa gari hilo ni matokeo ya juhudi za pamoja katika kuboresha huduma za afya. Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha kituo hicho kwa kuhakikisha kinapata watumishi wanaohitajika ili kiweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi