Wananchi wa Halmashauri ya Mji Kasulu wamehimizwa kufuga mbwa kwa kufuata sheria na taratibu za ufugaji bila kusahau haki za wanyama ambapo wanatakiwa kuhakikisha mnyama anapatiwa mahitaji muhimu kama vile chakula,banda,matibabu,chanjo na uhuru wa kuonesha tabia zao za asili, ili kulinda afya ya familia na jamii nzima.
Wito huo umetolewa na Mariot Paul Chikwela, Mratibu wa Chanjo za Mifugo wa Halmashauri ya Mji Kasulu, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani yaliyofanyika BaFULUMA Veterinary Clinic kata ya Nyansha. Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo: “CHUKUA HATUA SASA: WEWE, MIMI, JAMII” na yamefanyika kwa ushirikiano wa wataalam kutoka sekta za afya ya binadamu, mifugo na mazingira (One Health).
Bw. Chikwela ameeleza kuwa kichaa cha mbwa ni ugonjwa hatari usio na tiba, na mara tu mtu anapopata dalili zake hupelekea kifo. Ameonya wananchi kuepuka kuishi na mbwa wasiochanjwa na badala yake kuwafuga kwa mpangilio, ikiwa ni pamoja na kuwatunzia chakula, kuwapa makazi salama na kuhakikisha hawaachi kuzurura mitaani.
Kwa upande wake, Mtaalam wa Afya ya Binadamu John M. Wabike amesema maadhimisho haya hufanyika kila tarehe 28 Septemba duniani kote kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu (zoonotic diseases), ikiwemo kichaa cha mbwa ambacho kimekuwa chanzo cha vifo vingi vinavyoweza kuzuilika.
Wananchi walioshiriki wameishukuru Serikali kwa kutoa elimu na pia kuwapatia huduma ya chanjo ya mbwa bure, wakisema hatua hiyo itasaidia kulinda afya za kaya na kupunguza hofu ya kuenea kwa ugonjwa huo.