Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma imeanza maandalizi ya kuupokea mwenge wa uhuru kwa mwaka 2025 kwa kuboresha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika kikao kazi cha kujadili mikakati ya kuupokea mwenge wa uhuru kwa mwaka 2025 kilichowakutanisha viongozi na wakurugenzi wa halmashauri zote mbili mkuu wa wilaya ya Kasulu kanali Isaac mwakisu amesema wameanza mikakati mapema ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo itapitiwa na kukaguliwa na kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru mwaka huu.
"Mnatakiwa kusimamia miradi ya maendeleo kulingana na maelekezo yanayotolewa na Serikali na mnapohitaji kununua vifaa vya ujenzi hakikisheni anakuwepo afisa manunuzi ili aweze kununua vifaa vyenye ubora na kuhakikisha anapata risiti zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania na kuacha kununua risiti feki ambazo zinaweza kuleta changamoto wakati wa kutembelea miradi ya maendeleo" Amesema kanali Mwakisu.
Kwa wao baadhi ya wajumbe katika kikao hicho akiwemo mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii halmashauri ya mji Kasulu Bw.Nurfusi Aziz amepongeza hatua ya kuanza ufuatiliaji mapema na kwamba inalenga kuleta tija katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Tunashukuru kwa kikao hiki cha maandalizi na tunaamini wakaguzi kutoka mkoani Watatuelekeza vizuri katika miradi mbalimbali ili iweze kuwa na ufanisi na pia tumejipanga kuhakikisha tunapata vijana wengi wa hamasa ambao watashirikiana kuhakikisha kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa mwaka huu anaona na kutambua mchango wa vijana katika kuleta maendelo katika wilaya nzima ya Kasulu" amesema Aziz
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji Halamshauri ya Mji Kasulu Mwl vumilia Simbeye amesema atahakikisha fedha zinazotolewa na Serikali chini Ya Rais mh.Dkt Samia Suluhu Hassaan zinafanya kazi kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ubora.