Msingi wa utu na heshima kwa jamii ni upendo, amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye, wakati wa hafla ya makabidhiano ya viti mwendo 11 vilivyotolewa na Sauti Yetu Foundation kwa watoto na watu wenye mahitaji maalum, kwa ufadhili wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Hafla hiyo imefanyika katika Shule ya Sekondari Bogwe, Kasulu, ikihudhuriwa na viongozi wa serikali, wawakilishi wa taasisi mbalimbali, wazazi, na walezi.
Mwl. Simbeye amepongeza Sauti Yetu Foundation kwa moyo wa upendo na kujitolea kusaidia kundi hilo maalum, akisema:
“Tujenge jamii ya upendo kwa watu wenye mahitaji maalum. Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameonesha mfano bora, nasi tunapaswa kuendeleza moyo huu.”
Amehimiza wazazi na walezi kuwatoa na kuwawatambua watoto wenye mahitaji maalum ili wapate haki zao za msingi, na kuwataka taasisi kutoa taarifa kwa halmashauri ili kuwezesha uratibu wa huduma na mipango ya maendeleo.
Kaimu Mkurugenzi wa Sauti Yetu Foundation, Raphael Mabula, alisema mpango huo umeanzishwa ili kuwawezesha watu wenye mahitaji maalum kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Mwl. Simbeye pia alikumbusha kuhusu mikopo maalum isiyo na riba inayotolewa kwa watu wenye mahitaji maalum na kuwataka walengwa kuitumia kikamilifu.
Wazazi na walezi walishukuru msaada huo, akiwemo Amina Bakari aliyeeleza:
“Viti hivi vitawasaidia watoto wetu kuendelea na masomo na kushiriki ipasavyo katika jamii.”
Msaada huu ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikishwaji wa watu wenye mahitaji maalum katika shughuli za maendeleo na kuunda mazingira bora ya kujitegemea.