Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia Suluhu Hassan leo ametoa zawadi kwa vituo mbalimbali vya watoto waishio katika mazingira magumu nchini. Akikabidhi zawadi hizo kwa baadhi ya vituo vilivyopo Kasulu Mkuu wa Wilaya Kanal Isaack Anthon Mwakisu akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amesema amepokea zawadi ya chakula chenye thamani ya Tshs 2,500,000 kwa ajili ya Watoto waliopo Kasulu ili waweze kusherehekea vizuri sikukuu ya iddi.Kanal Mwakisu amesema amejisikia furaha sana kupata nafasi ya kufika na kukabidhi zawadi hizo ambazo zimetolewa na Mkuu wanchi kwa moyo wake wa upendo kwa wananchi wa hali zote na kusema ameagizwa kuwaambia Watoto kwamba Rais anawapenda na anawatakia sikukuu njema.Aidha DC Mwakisu amesema watoto kama hao wanahitaji faraja kutoka katika jamii ili waweze kukua wakitambua umuhimu wa kuishi kwa upendo na kuthamini wengine hasa walio katika mazingira kama wanayoyapitia. Kwa niaba ya watoto wote, mtoto mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa ametoa shukrani nyingi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia Suluhu Hassani kwa kutambua uwepo wao na kusema “...tumejisikia vizuri na kujiona wenye thamani kwa kutambuliwa na viongozi wakubwa ambao wana majukumu mengi lakini bado wamekumbuka uwepo wetu Mungu awabariki sana.Sasa tunaweza kujiona kama taifa kubwa la baadaye...”Aidha Mkurugenzi wa Mji Kasulu naye alisema kwamba wanamshukuru Mh Rais kupitia kwa Mkuu wa Mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya kwa zawadi hizo na kuwaasa wamiliki wa vituo hivyo kufikisha zawadi hizo kwa walengwa.Naye Kaimu Afisa ustawi kiongozi wa Halimashauri ya Mji ndugu Festo P.Solly aliongezea kwa kusema wanamshukuru sana Mh.Rais kwa kuendelea kuwashika mkono watoto hawa ambao wanahitaji sana upendo na kutoa wito kwa wamiliki wa vituo kuhakikisha wanawapa upendo watoto hawo na zaidi kwamba wao kama maafisa wanafurahi kufanya kazi kwa ushirikiano .