Mhe. Kanal Isack Anthony Mwakisu mkuu wa wilaya ya kasulu aongoza na kuungana na mamia ya watumishi wa serikali wilayani, viongozi wa chama Cha mapinduzi (CCM) pamoja na wakazi wa Kasulu Mjini katika kumbukizi ya siku ya Mashujaa nchini kwa kuwapa hamasa wakazi wa Kasulu katika kufanya usafi katika makazi yao.
Maadhimisho ya siku ya Mashujaa wilayani Kasulu yameanzia uwanja wa umoja uliopo katika kata ya Murubona na kuishia katika eneo la dampo lililopo maeneo ya mtaa wa Takukuru Kasulu mjini.Maadhimisho hayo yameambatana na ufanyaji usafi wa mazingira katika maeneo tofauti tofauti.
Aidha Mhe. Mkuu wa wilaya ameongea kuhusiana na siku ya kumbukizi ya mashujaa nchini. "Leo tupo hapa kwa ajiri ya kufanya usafi huku tukifanya kumbukizi ya siku ya mashujaa wetu nchini ambayo huwa inaadhimishwa kila tarehe 25, Julai kila mwaka. Waliomwaga damu, dada zetu, mama zetu, kaka zetu na baba zetu kutoka sehemu tofauti tofauti katika nchi hii zikiwemo na nchi jirani ambapo Tanzania iliongoza au ilishiriki katika ukombozi, Pia ni kumbukizi ya ndugu zetu waliomwaga damu katika kumng'oa Nduli Iddy Amini Dada huko Uganda. Hivyo serikali ilipanga kila tarehe 25 Julai iwe ni siku pekee ya kumbukizi ya mashujaa wetu nchini na sisi tumekutana mahali hapa ili kuadhimisha hilo".
Pia, Mhe.Mkuu wa wilaya ameeleza lengo na faida ya kufanya usafi "...Ni utamaduni kufanya baadhi ya shughuli ili kuzionyesha kwa wananchi, Sasa kwa eneo letu la Kasulu tuliona Kuna haja kubwa ya kufanya zoezi la usafi ili kuwapa hamasa wakazi wa Kasulu kuona faida na namna bora ya kufanya usafi katika maeneo yao, huku tukiadhimisha na kukumbuka mchango wa mashujaa wetu waliomwaga damu zao ili kuifanya nchi yetu na nchi jirani kuwa na amani na utulivu ..."
Maadhimisho ya siku ya mashujaa kitaifa yamefanyika Jijini Dodoma yakiongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa jamuhuri ya muungano.