Halmashauri ya Mji Kasulu imenufaika kwa kiwango kikubwa na mpango wa Shule Bora unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wa maendeleo kwa lengo la kuboresha elimu ya msingi nchini.
Katika mradi huu Halmashauri mwezi Januari 2025, imepokea kiasi cha shilingi milioni mia moja na Hamsini (150) za mafunzo ikiwemo mafunzo ya kusoma kuhesabu na kuandika (KKK), mafunzowezeshi ya utambuzi wa wanafunzi wenye mahitaji maalum ya kielimu.
Kupitia programu imewezesha eneo la ufundishaji na kujifunza mafunzo ya walimu mahiri wa somo la Hisabati na lugha ya kingereza yalitolewa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutumia mbinu shirikishi ambapo walimu wa masomo ya Hisabati na Kiingereza kutoka shule mbalimbali za msingi wameweza kutumia mbinu kama vile matumizi ya zana za kujifunzia ili kuweza kuwavutia watoto kujifunza kwa haraka mbali na njia za kuandika kwenye daftari tu kama ilivyozoeleka.
Katika mafunzo haya yaliyohudhuriwa na walimu takribani sitini na nne (64) wa shule za serikali ambapo imenufaisha walimu hao kuweza kutumia TEHAMA katika kujifunzia kama vile kompyuta na vishikwambi lakini pia nyimbo na katuni za kufundishia ambazo hutoa burudani na ujumbe maalumu.
Mpango huu umeleta matokeo Chanya ikiwemo uwezo wa walimu kufaragua zana za kufundishia hii imesaidia walimu kuweza kumudu darasa licha ya kuwa na wanafunzi wengi pamoja na kupunguza utoro
Watoto wenye mahitaji maalumu wamekua wakipitia changamoto mbali mbali katika kujifunza ikiwemo kusahaulika Pamoja na miondombinu kutokua rafiki lakini kupitia mpango huu umeweza kufundisha walimu na wadau kwanza namna ya kumtambua mtoto mwenye changamoto ikiwemo ulemamvu, changamoto ya magonjwa ya akili kama usonji. Imeweza kurahisisha ufundishaji wa Watoto hawa lakini pia kuwaweka karibu na kubaini hali zao wanazopitia.
Halmashauri ya Mji kasulu imefaidika kupitia mpango wa Shule Bora kwa kuwezesha mafunzo haya kwa wawezeshaji na walimu. Ambapo Mabadiliko yameonekana kwa wanafunzi wetu ni ushahidi wa wazi kuwa programu hii imeleta mafanikio makubwa.
Hapa mwezeshaji ngazi ya shule katika mafunzo wezeshi ya kutambua Watoto wenye mahitaji maalum ameeleza kuwa mafuzo hayo yana tija kwani itawezesha wanafunzi kupata afua stahiki wakati wa kujifunza pia ameleza itawezesha jaamii kuwa na elimu kuwaibua Watoto wanaoishi katika mazingira magumu wenye mahitaji maalumu ambao wamesahaulika.
Ushuhuda wa moja kwa moja umetolewa na Leokadia Emmanuel, mwanafunzi wa darasa la saba kutoka Shule ya Msingi Mwenda, ambaye amesema kuwa sasa wanaelewa vyema somo la hesabu kutokana na mbinu mpya zinazotumiwa na walimu wao.
“Mwalimu wetu anatufundisha hesabu kwa kutumia mfumo wa Gemin kutatua kanuni. Tunafurahia somo na tunalielewa vizuri zaidi kuliko awali,” amesema Leokadia kwa bashasha.
Mwalimu Frida Nakimu, kutoka Shule ya Msingi Murusi, ni miongoni mwa walimu waliopokea mafunzo hayo. Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutumia zana mbalimbali za kujifunzia na kufundishia, jambo lililosaidia kuongeza ushiriki wa wanafunzi darasani.
“Mafunzo tuliyopata yametufanya kuwa mahiri zaidi katika kufaragua zana na kuendesha vipindi vya darasani kwa ufanisi. Sasa somo la hisabati linapendwa sana na wanafunzi,” amesema Mwl. Frida.
Afisa Elimu Taaluma ambaye pia ni mratibu wa mpango huu bwana Shabani Baleka ameeleza kuwa kuna mipango thabiti iliyowekwa kuhakikisha kuwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia yanaimarika zaidi pamoja na kuinua taaluma kupunguza na kuondoa tatizo la kusoma kuandika na kuhesabu kuendelea kutumia teknolojia. Ambapo bajeti hiyo ya kiasi cha shilingi millioni 150 itasaidia katika miundombinu, vifaa vya kufundishia, na uendelezaji wa mafunzo kwa walimu.
Programu ya Shule Bora inaendelea kuwa kielelezo cha mafanikio ya ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika sekta ya elimu. Kupitia uwekezaji huu katika walimu, msingi wa elimu bora na endelevu umewekwa kwa vizazi vijavyo