Halmashauri ya Mji Kasulu imenufaika kwa kiwango kikubwa na mpango wa Shule Bora, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wa maendeleo, kwa lengo la kuboresha elimu ya msingi nchini. Kupitia programu hiyo, walimu wa masomo ya Hisabati na Kiingereza kutoka shule mbalimbali za msingi wamepatiwa mafunzo maalum yaliyojikita katika mbinu bora za ufundishaji, jambo lililoleta mabadiliko makubwa katika ujifunzaji wa wanafunzi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Vumilia J. Simbeye, ameishukuru Serikali kwa kuwezesha utekelezaji wa programu hiyo kupitia wadau wa Shule Bora, akisema imeleta mageuzi yenye tija katika mfumo wa utoaji wa elimu.
“Tunaishukuru Serikali kupitia wadau wa Shule Bora kwa kuwezesha mafunzo haya kwa walimu wetu. Mabadiliko tunayoyaona kwa wanafunzi wetu ni ushahidi wa wazi kuwa programu hii imeleta mafanikio makubwa,” amesema Mwl. Vumilia.
Ushuhuda wa moja kwa moja umetolewa na Leokadia Emmanuel, mwanafunzi wa darasa la saba kutoka Shule ya Msingi Mwenda, ambaye amesema kuwa sasa wanaelewa vyema somo la hesabu kutokana na mbinu mpya zinazotumiwa na walimu wao.
“Mwalimu wetu anatufundisha hesabu kwa kutumia mfumo wa Gemin kutatua kanuni. Tunafurahia somo na tunalielewa vizuri zaidi kuliko awali,” amesema Leokadia kwa bashasha.
Mwalimu Frida Nakimu, kutoka Shule ya Msingi Murusi, ni miongoni mwa walimu waliopokea mafunzo hayo. Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo wa kutumia zana mbalimbali za kujifunzia na kufundishia, jambo lililosaidia kuongeza ushiriki wa wanafunzi darasani.
“Mafunzo tuliyopata yametufanya kuwa mahiri zaidi katika kufaragua zana na kuendesha vipindi vya darasani kwa ufanisi. Sasa somo la hisabati linapendwa sana na wanafunzi,” amesema Mwl. Frida.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo, Bw. Julius Buberwa, amesema kuwa halmashauri imejipanga kuendeleza jitihada hizi kwa kutenga bajeti ya shilingi milioni 150 kwa ajili ya uboreshaji wa elimu ya msingi.
“Tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia yanaimarika zaidi. Bajeti hiyo itasaidia katika miundombinu, vifaa vya kufundishia, na uendelezaji wa walimu,” amesema Bw. Buberwa.
Programu ya Shule Bora inaendelea kuwa kielelezo cha mafanikio ya ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika sekta ya elimu. Kupitia uwekezaji huu katika walimu, msingi wa elimu bora na endelevu umewekwa kwa vizazi vijavyo.