Hayo yamesemwa leo na Kanal Michael Ngayalina Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe wakati wa Ufunguzi rasmi wa Kampeni ya Ugawaji wa Vyandarua vyenye dawa kwenye Kaya Kasulu TC iliyoanza rasmi hii leo kwa kikao kazi cha ulaghabishi na uhamasishaji kwa ngazi ya Halmashauri.
Katika kikao hicho Kanal Ngayalina amesema kampeni hii inafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais -TAMISEMI na Bohari ya dawa ambao ndiyo wasambazaji wa vyandarua, kwa ufadhili kutoka Mfuko wa pamoja wa afya (Global Fund) pamoja na mkoa wa Kigoma ambao ndio ugawaji huu unafanyika na hivyo amewashukuru wote kwa kufanikisha maandalizi na kuanza rasmi kwa kampeni ya ugawaji vyandarua kwenye kaya katika Halmashauri yetu
Aidha Kanal Ngayalina ameipongeza Halmashauri ya Mji Kasulu kwa kupiga hatua kubwa na kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya Malaria ambapo kiwango cha maambukizi ya Malaria kimepungua kwa karibu asilimia 45, kutoka asilimia 13.1 mwaka 2015 hadi asilimia 7.2 mwaka 2024; idadi ya wagonjwa waliothibitika kuwa na ugonjwa wa Malaria imepungua kwa asilimia 38 kutoka wagonjwa 20,472 mwaka 2015 hadi wagonjwa 12,524 mwaka 2024; na idadi ya vifo vitokanavyo na Malaria vimepungua kwa asilimia 71 kutoka vifo 113 mwaka 2015 hadi vifo 10 mwaka 2024. Napenda kuwashukuru sana wadau wote kwa kufanikisha kufikiwa kwa mafanikio haya.
“ Ningependa kutumia fursa hii kuwaasa wanajamii kutumia vyandarua wanavyopewa na kuendelea kulala ndani ya chandarua chenye dawa kila siku ili kujikinga na ugonjwa wa malaria. Matumizi yasiyofaa ya vyandarua yanarudisha nyuma mapambano dhidi ya malaria na kuleta athari kubwa ya kiuchumi Taifa letu.”
Mkuu huyo wa wilaya amewashukuru sana wadau wote wanaochangia katika mapambano dhidi ya Malaria, hapa nchini na hasa Mfuko wa Global fund wa kupambana na Malaria katika zoezi hili muhimu kwa Mkoa wetu wa Kigoma. Kipekee ameushukuru Mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (The Global Fund), Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania, Shirika la Afya Duniani (WHO), Taasisi ya ALMA na RBM Partnership to End Malaria, Taasisi ya Waheshimiwa Wabunge ya kupambana na Malaria – TAPAMA, Vyuo vikuu, Taasisi zisizo za Kiserikali, Sekta binafsi, Taasisi za Utafiti, wanahabari bila kusahau wananchi na jamii kwa ujumla kwa kuwa tayari kushiriki katika kutekeleza na kutumia afua zilizopendekezwa na Serikali kwa lengo la kuudhibiti na hatimaye kutokomeza ugonjwa wa malaria liza nchini.
“Ninaamini kuwa iwapo kila mmoja wetu atatekeleza wajibu wake ipasavyo na kuachana na tabia na mienendo isiyofaa, ambayo imekuwa ni kikwazo katika kutekeleza afua mbalimbali za kupambana na ugonjwa wa Malaria, Tanzania bila Malaria ifikapo mwaka 2030 inawezekana.“
.