Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu Mkoani Kigoma wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kupiga kura siku ya Jumatano tarehe 27/11/2024.
Akitoa taarifa ya zoezi hili la uandikishaji wa wapiga kura; Msimamizi wa Uchaguzi Mwalimu Vumila Julius Simbeye amesema zoezi la uandikishaji wa wapiga kura lilianza tarehe 11/10/2024 na kukamilika tarehe 20/10/2024 na kuchukua jumla ya siku kumi (10). Zoezi la Uandikishaji limefanyika katika Kata kumi na tano (15) zenye Tarafa mbili za Heru chini na Heru juu na kujumuisha vituo miamoja kumi na saba (117) vya kujiandisha kupiga kura.
Aidha, jumla ya wapiga kura Mia moja ishirini na tatu elfu miambili hamsini na nne (123,254) wamejiandikisha wakiwemo wanaume (ME) Hamsini na saba elfu miambili sabini na tano (57,275) wanawake (KE) sitini na tano elfu mia tisa sabini na tisa (65,979 ) sawa asilimia 101 Malengo yalikuwa ni kuandikisha wapiga kura Mia moja ishirini na mbili elfu na arobaini na mbili (122,042).
Vituo vya uandikishaji wa wapiga kura vilifunguliwa saa mbili kamili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili kamili jioni.
Uandikishaji huu umefanyika ili wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu waweze kupata fursa ya kumchagua Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na Wajumbe wake; kadiri ya Mwongozo wa Uchaguzi wa viongozi ngazi za Vijiji, Vitongoji na Mitaa uliotolewa Agosti, 2024 unavyoelekeza.
Orodha ya wapigakura itabandikwa leo tarehe 21/10/2024 kwenye mbao za matangazo na msimamizi wa uchaguzi ili kuwezezesha wananchi kukagua wapiga kura kwa ajili ya usahihi wa orodha hiyo, Kurekebisha jina la mpiga kura, kubadilisha taarifa iliyopo kwenye orodha hiyo na kufuta jina lililo orodheshwa kwa vile aliyeorodheshwa amekosa sifa za mpiga kura, zoezi la ukaguzi wa orodha ya wapiga kura litaendelea mpaka tarehe 27/10/2024 siku ya Jumatano.
Msimamizi wa Uchaguzi, Mwalimu Simbeye anawashukuru wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu kwa kujitokeza kwa wingi na kujiandisha ili waweze kupiga kura, amewasihi pia kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi tarehe 27/11/2024 ili kuwachagua viongozi wao watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano, Aidha anawashukuru kwa utulivu uliokuwepo kwa kipindi chote cha uadikishaji wa wapiga kura. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Kigoma, Mungu ibariki Halmashauri ya Mji Kasulu.